Aliyekuwa mwenyekiti wa LSK katika eneo la Bonde la ufa ametaka Idara ya Mahakama kufanyiwa mabadiliko zaidi.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akizungumza katika mahojiano ya kipekee afisini mwake na mwanahabari huyu siku ya Jumatatu, Bernard Ng'etich alisema kuwa in jambo la kusikitisha kuona kwamba kungali kuna mrundiko wa kesi katika mahakama za humu nchini.

Wakili huyo alisema kuwa hali hiyo imesababishwa na hatua ya baadhi ya mahakimu kuzembea kazini.

"Kando na mageuzi katika Idara ya Mahakama, bado kuna mengi ya kufanywa ikiwemo kupunguza mrundiko wa kesi mahakamani," alisema Ng'etich.

Wakati huo huo, alidokeza kuwa baadhi ya mahakimu wanafaa kuchunguzwa kwa kuzembea katika kutekeleza wajibu wao.

Wakili huyo alitoa wito kwa jaji mkuu Dr Willy Mutunga kuingilia kati swala hilo na kuwachukulia hatua wafanyikazi wa mahakama wanaozembea kazini.

"Jaji mkuu amejaribu lakini lingalikuwa jambo la busara iwapo angelitatua swala la mrundiko wa kesi linalochangiwa na mahakimu na majaji wazembe," alisema Ng'etich.

Aidha, alisema kuwa changamoto ingine inayoshuhudiwa ni kuwa baadhi ya kesi zinashughulikiwa na hakimu au jaji mmoja ambaye hulazimika kusafiri kila mara.

"Kwa mfano katika Mahakama ya Nakuru, kuna kesi nyingi ambazo hazijashughulikiwa jambo ambalo lafaa kutatuliwa,” alisema Ng'etich.

Haya yanajiri wakati Jaji mkuu Dr Willy Mutunga ametangaza kuondoka afisini kabla ya muda wake ili kuepuka mizozo ya kikatiba.