Kufuatia kubainika kuwa shillingi billioni 1 hazijulikani ziliko kutoka kwa hazina ya ustawishaji wa vijana, wakili Kemosi Mogaka amejitokeza kuitaka tume ya kukabili ufisadi nchini kuwakabili wahusika waliovuja mamillioni ya pesa kutoka kwa hazina hiyo. 

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akihutubia wanahabari mjini Nyamira siku ya Jumapili, Mogaka alisema kuwa yafaa tume ya kukabili ufisadi nchini iwachunguze na kuwachukulia hatua maafisa wakuu wa hazina hiyo. 

"Ni wajibu wa tume ya EACC kuwachunguza na kuwachukulia hatua kali za kisheria maafisa watakaopatikana kuhusika pakubwa kwenye uvujaji wa mamillioni ya pesa kutoka kwa hazina ya ustawishaji wa vijana," alisema Mogaka. 

Mogaka aidha aliitaka tume ya EACC kuwashurutisha wahusika wakuu kwenye sakata hiyo kurejesha mamillioni ya pesa zilizovujwa kutoka kwa hazina hiyo ya ustawishaji wa vijana. 

"Kuna watu wamezoea kupora pesa za umma na kisha EACC kukosa kuwachukulia hatua lakini kwa hili kosa la uvujaji wa pesa kutoka kwa hazina ya ustawishaji wa vijana, sharti watu waliohusika wawajibike na washurutishwe kurejesha pesa walizopora," aliongezea Kemosi.