Aliyekuwa mwenyekiti wa LSK Bonde la ufa wakili Bernard Kipkoech Ng'etich ametoa changamoto kwa wanawake katika taifa hili kuhakikisha wanashiriki katika nyanja za kisiasa kwa kuchaguliwa katika nyadhifa mbalimbali.
Katika mahojiano ya kipekee afisini mwake Jumatatu kuhusiana na mswada wa jinsia ambao wabunge walikosa kuupitisha, wakili Ngetich alisema kuwa ni jambo la kusikitisha kwamba mswada huo haukupitishwa.
Hata hivyo alisema kuwa ili kuepuka migogoro ya kikatiba kuhusiana na jinsia humu nchini, kuna umuhimu wa wanawake kujitosa kikamilifu katika ulingo wa kisiasa na kuhakikisha kwamba wanachaguliwa katika nafasi sawa na wanaume.
"Ni jambo la kusikitisha kwamba mswada huo wa jinsia haukupitishwa na wabunge lakini siwezi laumu wabunge bali langu ni kuwarai wanawake kujitosa katika siasa kikamilifu manake najua wanaweza hata kuchaguliwa katika nyadhifa mbalimbali za uongozi," alisema Wakili Ngetich.
Mwanasheria huyo kutoka Nakuru vile vile alitoa wito kwa jamii kwa jumla na hasa wanaume kuweka kando kasumaba yao ya kiume na kuhakikisha kwamba wanawaruhusu pia wanawake kushikilia nyadhifa mbalimbali za uchaguzi.
Matamshi yake yanajiri siku moja tu baada ya matamshi sawia kutolewa na Rais mstaafu Daniel arap Moi wakati alipokuwa mgeni wa heshima katika kongamano la akina mama wa Kanisa la AIC Milimani jijini Nairobi.
Moi alitoa wito kwa wanaume kuheshimu wanawake na kuwaruhusu kuwa na nyadhifa mbalimbali za kisiasa.