Wakili wa maswala ya kisheria Steve Mogaka amejitokeza kuitaka tume ya IEBC kuondoka afisini huku akisema wakenya wengi wamepoteza imani na tume hiyo.
Akiwahutubia wakazi wa eneo bunge la Mugirango Magharibi nyumbani kwake mjini Nyamira siku ya Jumapili, Mogaka alisema kuwa njia ya kipekee ya kuwahakikishia wakenya imani kwenye tume hiyo ni kuondoka afisini kwa makamishna husika.
"Njia ya kipekee kuwepo uchaguzi wa huru na haki mwakani ili viongozi wachaguliwe kwa haki ni sharti makamishna wa tume hiyo waondoke afisini," alisema Mogaka.
Mogaka aidha aliongeza kwa kuwarahi makamishna wa tume hiyo kuiheshimu katiba, huku pia akihimiza wananchi kuwachagua viongozi wachapa kazi.
"Wanalostahili kufanya makamishna wa tume ya IEBC ni kuondoka afisini kwa maana wakenya wamepoteza imani nao na yafaa waheshimu katiba, na ninawaomba wakenya wahakikishe kwamba wanawachagua viongozi wachapa kazi kwenye uchaguzi mkuu ujao," aliongezea Mogaka.
Ikumbukwe kuwa kwa muda sasa vigogo wa muungano wa Cord wamekuwa wakishinikiza tume hiyo kuondoka afisini.