Wakimbizi wa baada ya machafuko ya mwaka wa 2007/8 kutoka Kisii wamewasihi viongozi kutoka Kaunti ya Kisii kupigania haki yao ya kutaka kufidiwa Sh400,000 kama wakimbizi kutoka maeneo mengine.
Wakimbizi hao ambao walikuwa wakiongea na Mwandishi huyo nje ya uga wa michezo wa Gusii Alhamisi baada ya kumaliza mkutano wao wa kushauriana kuhusu kesi yao ambayo itatajwa mwezi ujao na kusikilizwa Julai.
Waathiriwa zaidi ya 300 kutoka maeneo mbali mbali ya Gusii wamewataka viongozi pamoja na Gavana James Ongwae kuwashughulikia ili kesi yao itatuliwe ipasavyo na kwa haraka.
Kupitia kwa msemaji wao Kasisi Nemwel Mokaya wakimbizi hao wamedai kuwa wakimbizi wengi ambao walifurushwa kutoka maeneo hasa ya Bonde la Ufa wamekumbwa na matatizo ya kifedha kwani wao walichomewa biashara zao, makaazi yao na kuachwa bila chochote.
"Tunataka kulipwa Sh400,000 kama wenzetu kutoka maeneo mengine ya Kenya ili tuweze kujiendeleza kiuchumi; tuna watoto wa kuenda shule na tulichotegea kama ukulima biashara zilichomwa na tukafurushwa. Sasa tunaishi kama wapangaji," alihoji msemaji Kasisi Mokaya.
Kesi ya wakimbizi hao ambayo ilikuwa isikilizwe wiki iliyopita ilifeli kung'oa nanga kwa sababu ya hakimu ambaye akishughulikia kesi hiyo Chrispine Nagila ilisemekana kuwa yupo Nairobi kwa shughuli rasmi.
Miongoni mwa madai waliyowasilisha mbele ya Mahakama hiyo ya Kisii ni pamoja na; kulipwa Sh400,000 kama wengine na pia kutatuliwa mzozo wa Sh25,000 ambazo inadaiwa zilitumiwa wakimbizi hao ambazo kwa mujibu wa msemaji wao hazikuwafikia wahusika hao.