Wakimbizi wa ndani kwa ndani wanaoishi katika eneo la Banita katika kaunti ndogo ya Nakuru Kaskazini wameelezea wasi wasi wao wa kulaghaiwa na kundi moja linalodai kuwa limepewa idhini na serikali ya kitaifa kushughulikia maswala ya wakimbizi wa ndani kwa ndani.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Hii ni baada ya kundi hilo kuzuru eneo la Banita mara kadhaa na kuwahadaa waathiriwa hao wa ghasia za mwaka wa 2007/08 kuwa serikali inalenga kuwapa fidia ya shilingi laki sita kila mmoja, lakini wanastahili kujisajili upya.

Akizungumza kwa niaba yao, Lucy Njeri, ambaye pia ni mshirikishi wa mtandao wa wakimbizi nchini katika kambi ya Gilgil na ambao walipokea fidia ya shilingi laki nne kutoka kwa serikali na shughuli zao zinalenga kuwatapeli waathiriwa wasiokuwa na ufahamu.

“Jana kundi hilo lilizuru eneo hilo na kuwafahamisha waathiriwa hao kuwa watasajiliwa upya. Waliwatoza shilingi 350 za picha kila mmoja na kuwaambia watalazimika kulipa shilingi elfu moja baadae,” alisema Njeri.

Mshirikishi huyo aliongeza kuwa serikali iliwasajili wakimbizi wote na kuanzisha harakati za kuwaondoa wale walio katika kambi na hakuna usajili mwingine unaoendelea.

“Wakimbizi wote wa ndani kwa ndani katika kanti ya Nakuru wanastahili kuwa makini wasianguke katika mtego huo wa utapeli. Pia tunaiomba serikali kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wanaowatapeli watu,” aliongezea Njeri.

Aidha, aliiomba kamati iliyobuniwa na serikali kufuatia kupitisha kwa sheria ya wakimbizi ya mwaka wa 2012 kushughulikia maswala ya wakimbizi kuharakisha kazi yake na kusuluhisha maswala ya wakimbizi kwani kuchelewa kwao kunatoa mwanya wa baadhi ya watu kuwatapeli wakimbizi hao.