Share news tips with us here at Hivisasa

Kundi la waathiriwa wa machafuko yaliyoshuhudiwa nchini punde tu baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007 kutoka eneo la Nyando, Kaunti ya Kisumu, limeitaka serikali kuwafidia.

Wakiongea na wanahabari siku ya Jumanne katika afisi ya naibu kamishna wilayani Nyando, waathiriwa hao wametoa wito kwa wabunge kutoka eneo la Nyanza kuingilia kati changamoto zinazowakabili ili wapate kufidiwa.

“Mimi ni mwathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007. Tumebaki bila chochote baada ya mali yetu kuharibika wakati huo na hivyo tunairai serikali kutusaidia,” alisema Benson Kimathi.

Waathiriwa hao walisema kuwa wanazidi kutaabika na kuitaka serikali kutatua shida zao kwa kuwafidia.

“Naomba serikali ituonee huruma kwa kuhakikisha imetusaidia sisi sote. Wengi wa walioathirika wamesalia na ulemavu hali ambayo imetatiza namna ya kujitafutia,” alisema Charles Tama.

Naibu kamishna wa Nyando Elizabeth Atemi, alisema serikali itaanza kuwashugulikia waathiriwa hao waliofikisha lalama zao katika afisi yake.

“Hawa ni wawakilishi wa wakimbizi wa ndani kwa ndani katika eneo la Nyando na wamewasilisha mapendekezo yao kwa Rais Uhuru Kenyatta kuhusu swala la kufidiwa kwa waathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007,” alisema Atemi.

Aliongeza, “Tumewaahidi kuwa tutawasaidia kwa kuwaonyesha mwelekeo wa kuendelea kutafuta fidia.”