Waathiriwa wa ndani kwa ndani wanaoishi katika eneo la Mai Mahiu wanakabiliwa na janga la kuhamishwa kwa mara ya pili, baada ya mvua kubwa ambayo ilinyesha sehemu hiyo  kuacha mitaro mikubwa ambayo  inahatarisha maisha. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Mitaro hiyo ambayo imesababishwa na mvua kubwa iliyonyesha mapema mwezi jana imewaacha wakazi hao kwa mshtuko na wasi wasi mkubwa.

Kambi iliyoathiriwa pakubwa ni ile ya Vumilai kando ya barabara kuu ya Naivasha kuelekea Mai Mahiu, ambapo zaidi ya familia mia moja zinakabiliwa na athari za kuhamishwa.

Mwenyekiti wa kambi hiyo Stephen Mbugua amesema kuwa shida hiyo ilianza mwezi Disemba ambapo mitaro hiyo ilianza kuchipuka, na sasa imepanuka na kufikia makazi yao.

"Wakati tulinunua hili shamba mvua haikuwepo, pahali hapa palikuwa tambarare. Kwa sababu janga la El-nino limetupata, serikali itusaidie kwa sababu kuna kamati iliundwa kuangazia madhara ya El-nino," alisema Mbugua.

Mkazi mmoja kwa jina Waweru Kimani alisema kuwa mitaro hiyo karibu inafikia makaburi matatu ya waathiriwa waliofariki yapata miaka minne iliyopita, na kuitaka serikali kufika eneo hilo ili kuwasaidia.