Vicar General wa Kanisa la Katoliki mjini Kisii Kasisi Jeremiah Nyakundi aliwaomba Wakristo na Waislamu kuungana pamoja ili kukashifu vitendo vya ugadi nchini bila kujali dini zao.
Kasisi Nyakundi alisema kuwa kuungana ndio njia mojawapo ya kuonyesha ushirikiano mwema kwa nchi haswa wakati shambulizi la ugaidi linapotokea kama lile lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Garissa na kuchukua uhai wa watu zaidi ya 147 na wengine kuachwa na majeraha mabaya.
Akiongea hapo siku ya Jumatatu katika hafla ya maombi ya wale wanafunzi kutoka Jimbo la Kisii waliouwawa kwenye shambulizi la kigaidi kule Garissa iliyofanyika katika uwanja wa Gusii, Kasisi Nyakundi aliwaomba Wakristo na Waislamu kukashifu vitendo vya ugaidi katika nchi ya Kenya na kuikumbuka nchi kwa maombi bila kulegea katika maombi hayo.
Pia alisema kuwa ugaidi ni janga ambalo limekumba Wakenya wote kwa jumla huku akisema kuwa Ukristo na Uislamu zote huwa zinahubiri amani na kuomba amani, jambo ambalo Kasisi Nyakundi alitaka liendelee kuonekana miongoni mwa wakenya wote na mtu asije akauawa kwa msingi wa dini au kutumia jina ya dini kutekeleza shambulizi ili kuaribia jina wengine.
“Ninawaomba ndugu zetu Waislamu kuungana pomoja na kukashfu kitendo hiki cha ugaidi ndiposa nchi yetu iendelee kusonga mbele kimaendeleo,” alisema Kasisi Nyakundi.
Kwingineko aliwaomba viongozi wote kuja pamoja wawe wa kitengo cha Kaunti au Serikali Kuu ili watafute suluhisho mwafaka la kupambana na ugaidi ambao umekita mizizi nchini huku akiomba Serikali Kuu hasa Sekta ya Usalama kuweka mikakati ya kuchukua hatua ya haraka na mapema ili kuokoa watu wakati shambulizi linatokea.
Hafla hiyo katika uga wa Gusii ilileta jamii ya Abagusii pamoja kwa maombolezo ya wanafunzi 12 kutoka Kaunti ya Kisii na 3 kutoka Kaunti ya Nyamira huku miili nane zikipelekwa katika uwanja huo siku ya Jumatatu.