Share news tips with us here at Hivisasa

Washikadau katika sekta ya pareto wameelezea wasiwasi kwamba Wakenya hawajakubali kurejesha imani yao katika kilimo cha pareto, licha ya juhudi za serikali kuu na za kaunti kufufua sekta hiyo.

Kulingana na washikadau, kati ya matatizo yanayofanya wakulima kutokumbatia kilimo hicho ni kutolipwa baada ya kupeleka mazao yao kwenye bodi ya pareto.

Mwenyekiti wa wakulima wa pareto nchini Justus Mwangi alisema kwamba ukosefu wa sera dhabiti  kuongoza ukuzaji wa pareto ni changamoto kuu kwa wakulima.

Ameongeza kuwa barabara mbovu na ukosefu wa mbegu kwa wakulima pia ni changamoto kuu.

Washikadau wengine akiwemo  Wachira Maina kutoka kampuni ya Highchem na afisa wa nyanjani wa kampuni hiyo Wilson Mwangi, walisema soko la bidhaa za pareto lipo tayari kimataifa, lakini pareto inayokuzwa Kenya ambapo kunapatikana kiwanda kikubwa zaidi cha pareto duniani, haiwezi kutosheleza mahitaji.

Wachira alisema serikali ya kitaifa imesaidia pakubwa katika kutafutia wakulima soko, kando na kufanya sekta hiyo ivutie ushindani wa sekta ya kibinafsi ili kurejesha imani kwa wakulima.

“Kwa sasa Highchem kama sekta ya kibinafsi tunaweza kuwanunulia wakulima pareto kwa sababu tumeshirikiana na bodi ya zao hilo. Kwa kilo moja ya zao hilo, tunanunua kwa shilingi 140 bei ya chini zaidi, na shilingi 375 bei ya juu zaidi kulingana na ubora wa zao lenyewe,” Wachira alisema.

Na huku pareto ikikuzwa katika kaunti 19 nchini, kubwa zaidi ikiwa ni kaunti ya Nakuru, Hilary Kamau kutoka wizara ya kilimo tawi la Nakuru, alisema kwamba wamefanikisha mradi wa kutoa mbegu kwa makundi ya wakulima katika kaunti ndogo nane za Kaunti ya Nakuru.

Washika dau hao walikuwa wakizungumza na mwandishi huyu mjini Nakuru Jumanne.