Wakulima wa jimbo la Kisii wameshauriwa kutumia mbinu za kisasa za kilimo ili kupata mazao mengi.
Akiongea afisini mwake, waziri wa kilimo kwenye kaunti hiyo Vincent Sagwe aliwataka wakulima kuiga mbinu za kisasa za kilimo kama njia moja ya kuongeza mazao.
“Nawahimiza wakulima kuanza kutumia mbinu mpya za kilimo kama njia moja ya kupata mazao Zaidi,” alisema Sagwe.
Aliongeza kuwa kufuatia kubadilika kwa hali ya anga na pia kupungua kwa rutuba kwenye udongo, ni muhimu kutumia mbinu mpya za ukulima kwani mbinu za jadi hazina uwezo wa kutoa mazao mengi.
“Kufuatia kubadilika kwa hali ya anga na kupungua kwa rutuba kwenye udongo ni vyema kutumia mbinu mpya za Kilimo ili kupata mazao zaidi,” aliongezea.
Vile vile, Sagwe amesema kuwa itakua vyema wakulima wakihudhuria kongamano za kilimo ambazo huandaliwa, kwa mfano maonyesho ya kilimo na hafla za kilimo zinazotayarishwa kwa ufadhili wa mashirika yasiyo ya kiserikali.
“Pia ni vyema kwa wakulima kuhudhuria kongamano na hafla za kilimo ambazo huandaliwa kwa minajili ya kuelimisha wakuliam kuhusu mbinu za kisasa za Kilimo,” alisema.
Aidha, waziri huyo amesema kuwa serikali ya kaunti ya Kisii ina mipango mahususi ya kuboresha kilimo na pia kuelimisha wakulima kuhusu mbinu za kisasa za kilimo.
“Kuna mipango mahususi ya kuboresha kilimo kwenye kaunti ambayo itawanufaisha Wakulima,” alisema.