Serikali ya jimbo la Nakuru itawekeza zaidi katika kilimo cha pareto kama hatua ya kwanza ya kufufua sekta hiyo ambayo iliporomoka na hadi sasa wakulima hawajarejelea kikamilifu kilimo hicho.

Share news tips with us here at Hivisasa

Waziri wa kilimo katika kaunti ya Nakuru Dr Stanley Chepkony amesema mikakati imekekwa ili kuhakikisha wakulima katika maeneo ambayo hukuza pareto wamepata mbegu tayari kwa msimu wa upanzi.

Amesema makundi ya wakulima katika kila wadi yatahusishwa katika mpango wa kupanda pareto ili kuhakikisha kuna miche ya kutosha ifikiapo mwezi Juni mwaka huu.

Chepkwony ambaye ameuliza wakulima kukubatia kilimo cha pareto amesema sekta hiyo itarejelea hadhi yake ya zamani baada ya serikali kuu na zile za kaunti ambazo hukuza zao hilo kuwekeza zaidi na kuhusisha wakulima katika mipango ya kufufua sekta hiyo.

Aidha waziri huyo amesema serikali ya jimbo itajihusisha na zoezi la kuwapa chanjo mifugo ili kuwakinga dhidi ya ugonjwa wa miguu na midomo.

Akiongea afisini mwake, Chepkwony amesema hatua hiyo imeafikiwa baada ya dalili za ugonjwa huo kuripotiwa katika maeneo ya Naivasha na Rongai.

Amesema wafugaji watalazimika kuchangia pamoja na kushirikiana na maafisa wa idara ya mifugo ili kufanikisha mpango huo.