Baadhi ya wakulima wa majani chai kutoka Ogembo wamelalamikia dhuluma ambayo inaendelezwa na makarani wa vituo vya kupima majani chai ambapo wakulima hao wanadai kumwagwa kwa majani hayo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wakulima waliokuwa wamepiga kambi kuchunga majani chai yao ya tangu Ijumaa, walilalamikia uongozo mbaya kutoka kwa viongozi wao wa kiwanda cha Tendere, ambao wamekuwa wakichelewesha kupima chai kwa muda ufaao ambapo huyamwaga majani hayo yakikaa kituoni zaidi ya siku mbili.

Jane Mogotu ambaye hupima majani yake kila wiki na kuuza majani yake kwa kiwanda cha Tendere aliutaka usimamizi wa kiwanda hicho kutilia maanani juhudi za wakulima za kuhangaika siku nzima kuchuma majani hayo na mwishowe kumwagiwa suala ambalo alitaja kuwa kero na la kuvunja moyo kwa wakulima wengine.

Samson Otara mmoja wa wakulima wa kiwanda hicho ambaye aliutaka uongozi wa kiwanda hicho kuwajali huku akisema kuwa majani chai uharibika yanapochelewa kukusanywa mapema na wanaohusika kwenye shughuli hiyo ya kupima na kupakia kwenye gari

"Kosa si letu ni la hawa wasimamizi ambao mara nyingi hufika kituoni wakiwa wamechelewa na kubeba baadhi ya majani na kuacha mengine ambapo wanaahidi kuja baadaye hali ambayo husababisha majani kukauka na kisha kuyamwaga majani chai hayo na kutupa hasara sisi wakulima," alisema Otara.

Hata hivyo juhudi za kutaka kuongea na mmoja wa wasimamizi wa kiwanda hicho kwenye simu hazifanikiwa.