Wakulima Mau-narok wamelalamikia ubovu wa barabara katika eneo hilo na kusema kuwa zimewasababishia hasara kubwa kwa kuwa imekuwa vigumu kwao kusafirisha mazao zao hadi sokoni.
Wakulima hao wamesema kuwa wanunuzi wa mazao ya shambani sasa wamesusia eneo hilo kutokana na obovu wa barabara ambazo hazipitiki.
Wakiongozwa na mwenyekiti wa chama ha wakulima wadogo wadogo mjini Mau-Narok, Stephen Kibet,wakulima hao walisema kuwa mvua inayonyesha imesababisha nyingi ya barabara kuharibika kiasi cha kutopitika kabisa.
Wakiongea katika kituo cha kibiashara cha Mau-Narok wakulima hao wamesema kuwa mazao yao ya mboga na matunda yanaozea shambani kwa kuwa wenye malori hawawezi kuingia vijijini kuyachukua.
“Mau-Narok inajulikana kama eneo la ukulima lakini tangu mvua ianze kunyesha tumekuwa na shida kubwa kwa sababu hatuwezi kusafirisha mazaokwenda sokoni na wenye malori hawawezi kuaj kuchukua kwa sababu barabara imeharibika kabisa,” alisema Kibet.
“Wale wachache wanoingia wanachukua mazao kwa bei duni kwa sababu wanasema wanapata hasara ya kukarabati magari yao yanayoharibikia barabarani,” aliongeza.
Kibet amemtaka gavana Kinuthia Mbugua kuzuru eneo hilo na kujionea kazi mbovu iliyofanywa na mwanakandarasi aliyepewa kazi ya kukarabati barabara hizo.
“Tunamtaka gavana Mbugua atufikirie sisi watu wa Mau-Narok kwa sababu tulimpa kura na afanye jambo hata kama atatumia pesa iliyotengwa kukabiliana na Elnino,” alisema Kibet.
Kibet alisema kuwa wakulima watawasilisha malalimishi yao kwa mwakilishi wadi wao ili ayafikishe kwa gavana Mbugua.