Share news tips with us here at Hivisasa

Wakulima wanaokuza zao la chai na wanaopeleka zao hilo kwenye kituo cha usagaji chai cha Nyansiongo wamepata sababu ya kutabasamu baada ya usimamizi wa kampuni hiyo kuwapokeza mbolea bila malipo.

Akihutubu katika eneo la Mwongori wakati wa kuwapokeza wakulima hao mbolea, mwenyekiti wa kiwanda hicho, Christopher Nyakora, alisema kuwa mpango huo utanufaisha wakulima wengi.

Nyakora alisema kuwa kampuni hiyo itatumia wakati huo kuwasajili wanachama wapya.

"Tuliamua kuwapokeza wakulima mbolea bila malipo sio eti kwasababu tunataka kuwarahi wakulima wengi kujiunga nasi, bali kuhakikisha wakulima wamepokezwa mbolea ili kuimarisha mazao yao,” alisema Nyakora.

Nyakora aidha aliongezea kuwa kando na usimamizi wa kampuni hiyo kuunga mkono ukuzaji wa zao la chai, vilevile inaunga mkono ukuzaji wa maharagwe na mahindi miongoni mwa wakulima.

"Ningependa kuwasihi wanachama wetu na wakulima walio na nia ya kujiunga nasi kutumia mbolea itakayosambaza kupanda maharagwe na mahindi, kwa maana tunahitaji kuona wakulima wasio tegemea tu zao la chai," alisema Nyakora.

Akizungumzia swala la baadhi ya wakulima kungoa zao lao la chai kwa kuwa zao hilo lilipata mapato ya chini kwenye malipo ya ziada mwaka jana, Nyakora aliwahimiza wakulima kutofanya hivyo.

Alisema kuwa ana matumaini kuwa zao hilo litaleta mapato ya kuridhisha mwaka huu.

"Ninajua kuwa baadhi ya wakulima wamekuwa wakingoa chai kwa kile wanachosema kuwa ni hasara. Kungoa mimea hiyo sio jambo zuri na ningependa kuwahimiza muendelee kukuza chai kwa kuwa ninatumai mapato ya zao hilo yataimarika mwaka huu. Tutakua tukiwapa mbolea kila baada ya miezi mitatu iwapo usimamizi wa kampuni utaidhinisha pendekezo letu," aliongezea Nyakora.