Wakulima wa majani chai katika vituo mbalimbali vya ununuzi wilayani Marani eneo bunge la Kitutu Chache Kaskazini wamelalamikia kutopimwa kwa zao na kusema wanapata hasara kubwa
Hii ni baada ya wakulima hao kusema majani chai yao hukaa kwa mda mrefu zaidi katika vituo hivyo na kupelekea kupata hasara kubwa kwani uzani hupungua zaidi wanapopima.
Sasa wakulima hao wameomba Halmashauri ya Uboreshaji wa Chai Kenya (KTDA) kupima na kuchukua majani chai kutoka kwa vituo hivyo kwa mda unaofaa ili kuzuia hasara hiyo.
Wakizungumza nasi siku ya Jumatano mjini Marani, wakulima hao wakiongozwa na Kennedy Onchiri na Solomon Makori walisema wakati mwingi uzani wa zao lao hupimwa baada ya siku mbili.
Jambo ambalo wamedai linaendelea kupawa hasara nyingi zaidi na wameomba halmashauri ya KTDA kufanya mageuzi kuhakikisha zao lao hupimwa kila siku.
“Huwa tunapata hasara nyingi maana hatupimi majani chai yetu kila siku," alisema Onchiri.
"Tunaomba makarani wa kupima zao letu wawe wanapima kila siku ili tusiwe tunapata hasara kila wakati,” aliongeza Onchiri.
Kulingana nao hii si mara ya kwanza wanalalamikia kutopimwa kwa zao lao na sasa wametishia kuuza zao hilo kwingine ikiwa KTDA haitafanya mabadiliko hayo kwa majuma mawili yajayo.