Huenda wakulima wa korosho katika eneo la Pwani wakanufaika baada ya Seneta wa kilifi Stewart Madzayo kuwasilisha ripoti ya namna kiwanda cha korosho kilivyosambaratika.
Kwenye ripoti yake Madzayo ametaka umma kuelezwa namna hisa asilimia sitini na tano zilivyotumika baada ya kiwanda hicho kuuzwa.
Seneta huyo alisema kuwa baada ya kuuzwa kwa kiwanda hicho, usimamizi wa kiwanda hicho haukutoa taarifa zozote zinazohusiana na hisa hizo zilikokwenda.
Alitaka uongozi huo kutoa taarifa kamili kuhusiana na swala hilo.
Wakati huo huo, Madzayo pia alisema kwamba wakulima wa zao hilo kwa sasa wamekosa imani na baadhi ya viongozi baada ya kuahidiwa kushughulikiwa matakwa yao na vyama vya ushirika.
Alisema kuwa mgogoro baina ya wakulima na kiwanda hicho ulizuka pindi tu baada ya kiwanda hicho cha korosho kilichojulikana kama Kenya Cushwenuts kuchukuliwa na kampuni ya Milenium Management.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya kilimo katika Bunge la Seneti Henry Ole Ndiema amesema kuwa kamati hiyo itatoa ripoti kamili ya namna kiwanda cha korosho kilivyosambaratika katika kaunti ya kilifi kwa muda wa wiki mbili zijazo.