Wakulima katika Wadi ya Nyota, eneo bunge la Kuresoi kaskazini wanaendelea kunung’unika wakisema hawajanufaika na mbolea inayotolewa na serikali kwa bei nafuu ili kuwezesha wakulima kuboresha usalama wa chakula nchini.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakulima hao wameteta kwamba serikali haikuwahusisha wananchi wakati wa kufunguliwa kwa vituo vya kusambazia mbolea hiyo wakisema vituo viwili vilivyofunguliwa katika eneo bunge hilo viko mbali na wananchi na huenda wengi wasiweze kunufaika.

Wametoa mfano wa kituo kilichofunguliwa katika eneo la Kiptororo hatua chache kutoka msitu wa Mau na kile kilichoko eneo la Kamara kama vituo vya kutoa mbolea, vituo ambavyo wamedai kuwa viko mbali wakiongeza kuwa huenda wakulima wakagharamika pakubwa wanaposafirisha mbolea kutoka hifadhi hizo.

Wenyeji hao wameelekeza kidole cha lawama kwa mbunge wa eneo hilo Moses Cheboi wakidai alishinikiza kufunguliwa kwa vituo hivyo katika ngome zake kwa lengo la kujinufaisha kisiasa.

Wamesema mwaka uliopita wakulima walishinikiza serikali kupitia kwa wasimamizi wa bohari la halimashauri ya nafaka na mazoa NCPD kufungua matawi yake katika kila Wadi ili kuwapa wakulima nafasi ya kunufaika na mbolea hiyo.

Kauli ya wakulima hao imeungwa mkono na MCA wa eneo hilo Njuguna Gichamu ambaye amesema wakulima wanategemea mbolea kutoka kwa serikali ili kuimarisha kilimo.

Gichamu amesema kwa niaba ya wananchi wa eneo hilo ataendelea kushinikiza serikali kusawazisha mgao wa pembejeo ili kutoa fursa kwa wakulima Mashinani ambao kwa kiwango kikubwa hujihusisha na kilimo biashara.