Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wakulima wa mazao ya mahindi kutoka katika kaunti ya Uasin Gishu wameonyesha kutoridhishwa kwao na bei ya mahindi iliyowekwa na serikali kuu hasa wizara ya kilimo.

Wakizungumza kwa vyombo vya habari hii leo, Wakulima hao wamesema kwamba bei hiyo ni ya chini zaidi na huwa inawaletea hasara kubwa na kuwa fedha wanazopata haziwezi kutosheleza mahitaji yao ya kila siku kama kulipa karo za wanafunzi.

Aidha walisema kwamba ikilinganishwa na fedha zinazotumika katika uzalishaji wa mazao hayo, bei hiyo ya mahindi huwapelekea kupata hasara kubwa kama wakulima wa zao hilo.

Vilevile, wakulima hao wameilaumu serikali kuu kwa kukosa kutoa fedha za kutosha zinazohitajika na bodi ya nafaka kununua mahindi, huku ikipelekea kulemazwa kwa shughuli za uuzaji mahindi hayo.

Wamezidi kulalamikia kiwango kidogo cha fedha zilizotolewa na serikali, huku wakisema kwamba bajeti iliotolewa na serikali iliwapa shilingi bilioni mbili na milioni mia saba pesa taslimu, kinyume na shilingi bilioni kumi ambazo zinazohitajika kuyanunua mahindi hayo.

Kwa upande mwingine, mkurugenzi wa wa chama cha wakulima eneo la Northrift Kipkorir Menjo aliwaunga mkono wakulima hao, huku akihimiza serikali kujitokeza na madawa ya kukabili ugonjwa wa mimea ya mahindi unaosambaa kwa kasi kwa kabla ya kusababisha madhara mengi zaidi.