Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Chama cha wakulima wa majani chai cha 'Gucha Alliance' kimekosoa usimamizi wa viwanda vya majani chai katika eneo hilo kwa kununua mashine za kusaga majani chai bila kuwahusisha.

Wakulima hao walisema kuwa waliwekewa gharama ya kulipia mashine hizo ilhali hawakuhusishwa wakati wa ununuzi.

Wakizungumza na waandishi wa habari siku ya Ijumaa katika eneo la Gucha, wakulima hao wakiongozwa na mshauri mkuu wa chama hicho Nyamwange Oigara, walisema wamekuwa wakilipia mashine hizo kwa muda mrefu.

Oigara alimwomba Gavana wa Kaunti ya Kisii James Ongwae na waziri wa kilimo katika kaunti hiyo Vincent Sagwe kuingila kati swala hilo na kuwasaidia.

“Sisi kama wakulima wa majani chai tumekuwa tukisumbuka kwa muda mrefu kufuatia usimamizi wa viwanda, maana wasimamizi hao wanaenda wanaleta bidhaa mbalimbali ikiwemo mashine za kusaga majani chai bila kutujulisha na kutusukumia gharama ya bidhaa hizo,” alisema Oigara.

Aliongeza “Tunaomba gavana na waziri wa kilimo wajitokeze waonane na wakulima tuwape malalamishi yetu.”

Aidha, Charles Nyang’wara, mkulima wa majani chai, aliwaomba wasimamizi wa viwanda hivyo kujulisha wakulima wanachohitaji kununua kabla ya kufanya hivyo ili kuzuia wakulima kulipa madeni ambayo hawajui yalikotoka.

“Wameleta mashine bila sisi kujulishwa na sasa wamesema tutakatwa pesa kutoka zile pesa za ziada. Hiyo ni hasara kwetu,” alisema Nyangw’ara.