Wakulima wa majani chai kutoka Tendere, wilaya ya Ogembo kaunti ya Kisii wameombwa wasing'oe zao hilo na kupanda michai ya gredi 1 ili kuimarisha bei ya zao hilo ambayo inafifia.
Hii ni mojawapo ya harakati za kufufua matumaini ya wakulima wengi wa zao hilo, ambao wamekuwa wakiling'oa huku wakilalamikia malipo duni kutokana na zao la majani chai.
Kwenye mahojiano na mwenyekiti wa vituo vya kupima majani chai vya kiwanda cha kusaga majani chai cha Tendere kilichoko Ogembo, John Nyabuto aliwaomba wakulima wa eneo hilo kuacha kung’oa zao hilo na kuanza kushiriki makongamano yanayoandaliwa na kamati kutoka idara ya kilimo na kufaidi utaalamu jinsi ya kupanda mazao ya ubora wa juu.
“Tuwe wakulima wenye ujuzi kwa kuhudhuria hafla za mafunzo ya wataalamu wa kilimo, hivyo tutajikimu vizuri kwa shughuli za kilimo cha majani chai,” alisema mwenyekiti huyo.
Kilimo cha majani chai kimekuwa kikififia kwa siku za hivi karibuni kwenye maeneo mengi ya Kisii na Nyamira, ambapo wengi wa wakulima wa maeneo hayo wamehiari kuanza kung’oa mimea yao, na kuingilia kilimo tofauti na kushtumu usimamizi wa mamlaka majani chai nchini kuwadhulumu.