Wakulima kutoka eneo la Muhoroni wametishia kutopeleka zao lao katika kiwanda cha kutengeza sukari cha Muhoroni.
Hatua hiyo inajiri baada ya wakulima hao kudai kuwa kampuni hiyo imekosa kuwalipa pesa zao tangu mwaka jana Oktoba hadi leo.
Wakizungumza siku ya Jumatano, wakulima hao, wakiongozwa na katibu mkuu wa chama hicho cha wakulima, Noah Opiyo, walisema kuwa wametoa makataa ya muda wa wiki mbili na endapo hawatalipwa, basi hawatawahi peleka miwa yao katika kiwanda hicho.
Opiyo alisema kuwa wakulima husika watachukua hatua za kisheria dhidi ya kampuni hiyo, iwapo hawatalipwa fedha zao.
''Iwapo kampuni hiyo itashindwa kuwalipa wakulima pesa zao, basi swala hili itabidi litatuliwe mahakamani,'' alisema Opiyo.