Wakulima wa mmea wa nazi katika kaunti ndogo ya Rabai wamelalamikia ukosefu wa soko wa bidhaa hiyo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wakulima hao walisema kuwa ukosefu huo wa soko umechangia katika wao kuwa maskini.

Wakizungumza huko Rabai siku ya Jumatatu, wakulima hao waliitaka Wizara ya Kilimo kuwatafutia soko nzuri hapa nchini na hata katika nchi za nje ili waweze kuuza bidhaa hiyo kwa wingi.

Kulingana na mwenyekiti wa kikundi kimoja cha kina mama katika eneo hilo, Sidi Khasim, shirika la kijamii linalowatafutia soko wakulima hao lilisema kuwa panahaja ya serikali kuwatafutia soko kubwa, kwa kuwa wakulima hao wanapata mazoa bora na ambayo yanaweza kupata soko zuri katika nchi za nje.

Kulingana na mwenyekiti wa kamati ya kilimo kaunti ndogo ya Rabai Said Hamisi, wakulima wa nazi hawajatafutiwa soko kwa muda mrefu, jambo ambalo amelitaja kuwapa muda mgumu.

Alisema kuwa sekta ya ukulima imejaribu kila iwezavyo kuwatafutia soko katika eneo la Pwani lakini mgawanyiko miongoni mwa wakulima na kutokuwa tayari kuungana katika makundi ya wakulima wanaozalisha bidhaa moja ndio changamoto kuu.

Aidha, Hamisi alisema kuwa ipo haja ya wakulima wote kujiunga na makundi ili kurahisisha kazi kwa sekta ya kilimo.

Mama Magret Kanze, ambaye huuza bidhaa za mnazi kama vile nazi, pombe ya mnazi na mbao, alisema kuwa kwa sasa hali imebadilika, huku akiongeza kuwa biashara ambayo iko imara kwa sasa ni ile ya mbao.

Bi Kanze alisema kuwa hali hiyo itakuwa hatari kwani itawalazimu kukata mimea jambo ambalo alisema litaathiri uzalishaji wa nazi na hata pombe hiyo ya mnazi.

Wakulima hao aidha wameitaka mamlaka ya maendeleo ya ukulima wa mmea wa mnazi kushughulikia swala hilo kwa kufikisha maombi yao kwa viongozi kwani kwa sasa wameishia kukadiria hasara kubwa.

Wakulima hao wamemtaka Mbunge wa Kaloleni Gunga Mwinga kuliangazia swala hilo kwa uzito kwani wengi wa wazazi katika eneo hilo wanategemea mazao hayo kukimu mahitaji ya familia zao.