Wakulima wa zao la nyanya Subukia kaunti ya Nakuru wanaitaka serikali iwekeze katika ukulima wa nyanya kwa kujenga kiwanda kwenye kaunti ya Nakuru.
Wakulima hao walisema kwa sasa wanazidi kupitia changamoto nyingi kutokana na ukosefu wa soko nzuri la zao hilo.
“Kuanzia miaka ya tisini wakati ambapo kiwanda cha Kenylon kilifungwa, wakulima hapa wamekuwa wakiteseka tu. Hatuna soko la nyanya kabisa,” Josephine Nyambura alisema.
Nyambura alisema wakulima wengi kwa sasa wanalazimika kuwacha zao lao liharibike.
“Serikali irudishe kiwanda cha nyanya hapa ili tufaidike,” Nyambura aliongeza.
Wengi wa wakaazi wa Eneo la Subukia wanashiriki kilimo cha nyanya kwa kutumia maji ya mto Subukia.
“Nyanya hapa zinafanya vizuri sana, lakini hakuna mkulima atazidi kushiriki kilimo hiki bila ya matokeo mazuri. Kwa sasa hatupati soko mwafaka,” Peter Nderitu alisema.