Wakulima wa Pareto wa eneo la Karate mjini Naivasha sasa wameelekea kortini kupinga ujenzi wa zahanati moja eneo la Kinamba kwenye ardhi tata mjini humo.
Kwenye barua ya dharura, wakulima hao wanataka mahakama kuagiza kusimamishwa kwa ujenzi huo ambao unafadhiliwa na hazina ya CDF ya mji huo.
Wakili wa wakulima hao George Kimani amesema kuwa ardhi inayojengewa zahanati hiyo ni mali ya wakulima hao na haijawahi kuuzwa.
Kimani amekinyoshea kidole cha lawama mbunge wa sehemu hiyo John Kihagi kwa kutumia pesa za umma visivyofaa kwani hakuna siku hata moja wakulima hao walikutana na kuamua kuuza kipande hicho cha ardhi.
Kiongozi mmoja mjini humo Charles Mburu amemzomea mbunge huyo na kutaka kuchunguzwa kwa miradi yote ambayo imefanywa na hazina hiyo tangu mwaka wa 2003.
"Hazina ya CDF Naivasha haijatekeleza malengo yake kikamilifu na tunaitaka vile vile tume ya kupambana na ufisadi nchini EACC kufika eneo hili na kufanya uchunguzi wao maanake kuna ubadhirifu katika hazina hiyo hapa Naivasha," alisema Mburu.