Wakulima wa viazi katika eneo la Kuresoi, Kaunti ya Nakuru wameelezea kukerwa na riporti kuwa baadhi ya wakulima wameelekea Mahakamani kupinga mfumo wa upakiaji wa kilo 50 za gunia la viazi wakiunga mkono mfumo wa zamani wa kilo 110.
Wakiongozwa na Kipkorir Koslei, wakulima hao waliwalaumu madalali wa uuzaji wa viazi wanaodai ni wakulima kwa tatizo lilioko wakisema kuwa ni makosa kupinga agizo la Serikali la upakiaji wa viazi kutoka kilo 50 hadi 110 zamani ambazo walisema zilikuwa zinawapunja wakulima.
Wakulima hao wa viazi walikuwa wakiongea katika uwanja wa Teta kule Kuresoi katika hafla iliyo wakutanisha.
Wakulima hao wamesema kuwa mmea huo umewasaidia kulipa karo ya watoto wao pamoja na kuwasaidia kujimudu kimaisha.
Waliongeza kuwa viazi hukua kwa muda mfupi kukomaa ikilinganishwa na mimea nyingine, basi ndio maana wanaitegemea sana.
Kwa sasa bei ya debe moja la viazi huuzwa kwa Sh800 na wakulima wamefurahia bei hiyo mpya ambazo zinatarajiwa kushuka kwa kipindi cha miezi mitatu ijayo kutokana na mvua inayoendelea kunyesha kwa sasa hivi.
Serikali kupitia kwa Wizara ya Kilimo ilitoa ilani kwa yeyote atakaye patikana amekiuka sheria ya uuzaji wa kilo 50 za upakiaji wa viazi kuchukuliwa hatua kwa sababu sheria hiyo inalenga kuwaruzuku wakulima hao kutoka kwa unyanyasaji wa madalali.