Wakulima wa majani chai wa kituo cha eneo la Kebobora kilichoko eneo Bunge la Bobasi katika Kaunti ya Kisii wamelalamikia wizi ambao unatekelezwa na baadhi ya wakulima wenzao kupima majani chai yao wakati hawapo na kuhesabiwa kilo zisizo zao.
Wakizungumza na Mwandishi huyu siku ya Jumapili katika eneo hilo la Kebobora, wakulima hao walisema baadhi ya wakulima wenzao hupima majani chai yao wakati hawapo na kuhesabiwa kilo za wengine.
“Gari la kupima majani chai ilikuja usiku na sikuwa karibu nikapigiwa simu niende kupima majani chai hayo nilipofika nikapata hakuna majani chai yangu kumanisha kuna wakulima wengine wanaendelea na wizi wa majani chai,” alihoji Samson Ongori mkulima wa majani chai katika eneo la Kebobora.
“Nilichukua muda wangu kuchuna majani chai shambani na sasa nashindwa nitafanya nini kufuatia hasara yenye tayari nimesababishiwa. Tunaomba wanakamati watafute suluhu kuhusiana na wizi huo wa majani chai katika kituo hiki maanake sio mimi wala wawili wamepoteza majani chai ya, ni watu kadhaa huwa wanapoteza majani yao kwa njia hizi zisizo za kihalali,” aliongezea Ongori.
Kamati ya kituo hicho cha Kebobora wameombwa kutafuta suluhu kuhusiana na wizi wa majani chai ya wakulima wengine ili wanao tabia hiyo wasije wakaendelee na tabia hiyo mbaya.
“Tunaomba kamati iingilie kati mambo hayo kwani twasumbuka sana kungojea gari kwa muda mrefu na pale wahusika wanapojua kuwa hawatafika, inafaa wafunge kwa kufuli kituo hiki ndio tusipoteze majani chai yetu,” alisema Ongori.
“Inastahili wahusika watafute mbinu mbadala ya kuhakikisha kila mkulima aliyepeleka majani chai amefika ili kupima kilo zake na hiyo itakuwa suluhu mwafaka, sio eti wengine wanapima na kupotea na pesa za wenzao,” alisema Beatrice Kenani mkulima mwingine aliyeathiriwa na wizi huo.