Zaidi ya wakulima 20 kutoka kijiji cha Kemanko Lokesheni ya Mwamonari, eneo Bunge la Kitutu Chache Kaskazini katika Kaunti ya Kisii wanaendelea kupata hasara kubwa kutokana na mvua inayoendelea kunyesha kote nchini.
Wakulima hao wamekabilia hasara kufuatia mmomonyoko wa udongo ambao ulikokokoa mbegu za mahindi, mharagwe na wimbi waliokuwa washapanda tayari kutoka mashamba yao siku ya Jumanne.
Wakiongea na Mwandishi huyu wa Habari siku ya Jumanne katika kijiji hicho Esther Ombaki, Patric Mecha na Evans Onsakia walisema mvua hiyo ilisomba mbegu yao waliopanda ambayo iliwagharimu pesa nyingi kununua mbegu hizo pamoja na mbolea na kuachwa vinywa wazi na kushindwa la kufanya.
Wakulima hao wakiongozwa na Patric Mecha wameiomba Serikali ya Kaunti ya Kisii kuwasaidia kwa kuwanunulia mbolea au kuwapunguzia bei ya mbegu na mbolea kwani gharama ya mbolea imepanda bei kwa kiasi kikubwa watakapoanza kupand tena baada ya mvua hiyo kuharibu shamba lao.
“Tunaomba Serikali itupunguzia bei ya mbolea ili tupande tena na tusije tukakabiliwa na njaa,” alisema Mecha.
Mvua hiyo ambayo imewasababishia hasara hiyo imenyesha kwa mwezi mmoja sasa. Wakulima hao kwa sasa wamesihi Serikali kufanya kila iwezalo kuwapunguzia bei ya mbolea na mbegu baada ya bei hizo kupanda juu zaidi msimu huu wa upanzi.
Bei ya mbegu kilo mbili ni Sh350 ambayo ilipanda kutoka Sh250 na bei ya mbolea nayo kilo hamsini ni Sh3,500 kutoka Sh2,700 bei ya hapo mbeleni.