Mwenyekiti wa chama cha Kenya Social Congress katika eneo la Kisii Atati Kengere amewaomba Wakurugenzi wa viwanda vya majani chai vilioko katika Kaunti ya Nyamira na Kisii kuweka mikakati kabambe ya kuhakikisha majani chai yamepimwa uzani wakati ufao.
Akiongea na Waandishi wa Habari siku ya Jumatatu katika mji wa Nyamira, Mwenyekiti Kengere alisema kuwa wakulima wa majani chai hupata hasara kubwa wakati hawapimi uzani wa majani chai yao kwa wakati ufaao.
“Wakulima wa majani chai husumbuka sana wanapokuwa kwa nyumba za kuuza majani chai hayo wakisubiri kupimwa kwa uzani wa majani chai kwa zaidi ya siku tatu mfululizo na kuwasababishia kupata hasara kubwa maanake majani hayo yakichukua muda kabla ya kupimwa hupoteza uzani kwa asilimia kubwa,” alihoji Kengere.
Mwenyekiti Kengere aliwaomba Wakurugenzi kuhakikishe wakulima hao hawapati hasara kwani wengi wao hutegemea ukulima huo na hata kuwasomesha watoto wao.
Kulingana na utafiti uliofanywa na Mwandishi huyu wa Habari, eneo Bunge la Kitutu Masaba ndio sehemu ambayo imekumbwa na changamoto hiyo kwa wakulima kwa kutopima majani chai yao kwa zaidi ya siku tatu wakishinda kwa nyumba za kuuza majani chai na kupata hasara kubwa.
Wakati uo huo, Mwenyekiti huyo ameiomba Serikali ya Kaunti ya Nyamira kuzikarabati barabara zote za zilizoko katika Kaunti hiyo ili kurahisisha uchukuzi wa majani chai kutoka nyumba za kuuza majani chai hayo.