Wakuu wa idara katika serikali ya Kaunti ya Nyamira wameonya dhidi yakukataa kuitikia wito wakujiwasilisha mbele ya kamati mbalimbali za bunge ambazo huwa na nia yakuchunguza maswala fulani yanayokabili idara husika.
Akihutubia kikao cha wanahabari afisini mwake siku ya Alhamisi, spika wa bunge la Kaunti ya Nyamira Joash Nyamoko alisema kuwa wakuu wengi wa idara mbalimbali wamekuwa na mazoea yakukwepa wito yakutakiwa kufika mbele ya kamati mbalimbali za bunge la kaunti hiyo.
Alisema kuwa wasimamizi hao huwatuma wadogo wao kufika mbele ya kamati hizo huku akiongezea kuwa hali hiyo hupelekea kamati za bunge kupeana ripoti zisizo zakuridhisha kuhusiana na maswala fulani.
"Mbinu zetu za uongozi ni wazi na sharti wasimamizi wa idara mbalimbali katika serikali ya kaunti hii waheshimu hilo kwa kujiwasilisha mbele ya kamati za bunge ili kujibu shtuma zinazokabili idara zao,” alisema Nyamoko.
Nyamoko alisema kuwa tayari amewaandikia barua Gavana John Nyagarama na katibu wa serikali ya kaunti hiyo Erick Onchana, barua yakuwataka wasimamizi hao kujiwasilisha mbele ya kamati za bunge kulingana na sheria zilizopo.
"Majukumu yetu ya uangalizi yatafeli pakubwa ikiwa wasimamizi wa idara mbalimbali wataendelea kufeli kujiwasilisha mbele ya kamati za bunge. Tayari nimemwandikia Gavana Nyagarama na katibu Aori barua zakuwataka kuwashurutisha wakuu hao kujiwasilisha mbele ya kamati za bunge kwa kuwa bunge hili linawajibikia umma na sharti tutekeleze majukumu yetu,” alisema Nyamoko.
Nyamoko alisema kwamba ripoti mbalimbali za baadhi ya kamati za bunge hukataliwa bungeni kwasababu ya kuwa hafifu au kutokamilika kutokana na wakuu hao kukataa kufika mbele ya kamati za bunge kujibu maswali.
"Tunataka kuepuka visa ambapo ripoti za kamati mbalimbali hukataliwa kwenye bunge hili na sharti kamati hizo ziheshimiwe. Kama spika lazima nitekeleze wajibu wangu kwa kuhakikisha nimewaarifu maafisa wakuu serikalini kuhusiana na swala hili,” alisema Nyamoko.