Viongozi wa makanisa eneo la Nyakach wameitaka Serikali kutilia maanani sheria za mahakama ambapo mtu yeyote anayekabiliwa na hatia kushitakiwa kwa muda wa masaa 24 kwa mujibu wa sheria za mahakama nchini.
Kupitia kwa mkutano wa viongozi wa muungano wa makanisa katika eneo la Nyakach, viongozi wakuu wa muungano huo waliitaka Serikali kuzingatia sheria iwapo inataka kizazi chenye maadili nchini.
Walisema kuwa sheria inaboresha jamii kama inatumiwa vyema na kuongeza kuwa inasambaratisha uzalendo iwapo haizingatiwi vikamilifu.
Mhubiri Solomon Abogo wa Kanisa la SDA ambaye ni mwenyekiti wa muungano huo alisema kwamba kuna visa ambapo washukiwa wengi hukaa kizuizini kwa siku nyingi bila kufunguliwa mashtaka, hali ambayo alisema kuwa inaleta uhasama miongoni mwa jamii nyingi.
“Tunataka iwapo mtu atakamatwa kwa madai fulani kupelekwa mahakamani haraka iwezekanavyo kwa muda wa masaa 24 na wala siyo kuzuiliwa na kuteshwa kwa zaidi ya siku moja, mbili,” alisema Mhubiri Abogo.
Viongozi hao walitaja kisa ambapo kijana mmoja kutoka katika jamii ya waumini walio kwenye muungano huo alikamatwa mwezi mmoja uliopita na akaendelea kuzuiliwa bila kupelekwa mahakamani kufunguliwa mashtaka.
“Tumegundua kwamba kuna mahaka za siri zinazoendeshwa chini kwa chini kwenye vizuizi vya Polisi. Watu wanakamatwa hata bila hatia na kuendelea kunyanyaswa bila kushtakiwa, kisa na maana mtu atoe pesa ndipo aachiliwe hata kama hana makosa,” alidai Jonathan Osore aliye katibu wa muungano huo.
Aidha viongozi hao walimtaka Rais Uhuru Kenyatta kukaza kamba katika kupambana na ufisadi, wakimtaka kunyosha mjeledi huo kwa kila yeyote atakayepatikana na hatia na wala usiwe tu mtego uliowekwa kunasa samaki wadogo pekee katika bahari ya Papa na Nyangumi.