Wakuu wa shule za msingi katika eneo la Chemelili wameombwa kuimarisha na kuboresha mazingira ya shule zao kwa usalama na manufaa ya wanafunzi.
Wazazi kwenye Shule ya Msingi ya Mwangazi katika Tarafa ya Chemelili wamewataka wakuu wa shule kwenye eneo hilo kuzingira shule zao kwa kuweka uwa ili kuzuia wanafunzi kuruka nje ya uwanja wa shule wakati usiyofaa.
Wazazi hao ambao majuma machache yaliyopita walishinikiza kamati ya maendeleo ya shule hiyo kuweka uwa kuzingira shule hiyo, waliwataka majirani wao pia kufanya vivyo hivyo kwenye shule zote zilizowazi katika eneo hilo.
“Tunahitaji shule zote za eneo hili kuzingirwa na uwa ili kuwahakikishia wanafunzi usalama na hata kupunguza visa vya utovu wa nidhamu ambapo wanafunzi huruka nje ya uwanja wa shule wakati usiyofaa,” alisema Jacob Obonyo mmoja wa wazazi hao.
Wazazi hao ambao walikua wakihutubu kwenye mkutano wa walimu na washikadau ambao uliandaliwa shuleni humo siku ya Alhamisi waliwataka walimu wakuu kushirikiana na Kamati ya wazazi inayoongoza mipango ya maendeleo ya shule kushirikiana ili kurahizisha maendeo na kudhibiti usalama wa wanafunzi wao.
“Bila ushirikiano hatuvuni chochote hapa. Hivyo basi tunatoa kauli yetu kama wazazi kwamba kuweko na ushirikiano katika utendakazi shuleni humu ili kuboresha mazingira na elimu ya watoto wetu,” alisema Nancy Nyaoro mzazi.
Shule nyingi za Kanda hiyo ziko katika maeneo ya barabara ambapo wanafunzi kila wakati hupatikana wakiwa nje ya shule kwa kuvutiwa na magari na tingatinga za kubeba miwa ambazo hupitapita kila wakati.