Serikali ya kitaifa na ile ya Kaunti ya Mombasa zimetakiwa kuwa mstari wa mbele katika kushughulikia maslahi ya watu wanaoishi na ulemavu Mombasa.
Akizungumza siku ya Jumatano mjini Mombasa, mwakilishi wa watu wanaosihi na ulemavu Naftali Swaka, alisema kuwa walemavu wametengwa sana.
“Watu wanaoishi na ulemavu wamenyimwa haki zao kwa kuwa huwa hawachukuliwi kama binadamu wengine wa kawaida,” alisema Swaka.
Mwakilishi huyo alisema kuwa kuna idadi kubwa ya walemavu jijini Mombasa ambao wamesahulika na hawahusishwi katika maswala ya maendeleo, jambo linalowafanya wengi kujihusisha na shughuli ya kuombaomba jijini.
Swaka aliiomba serikali kutilia maanani swala la watu wanaoishi na ulemavu na kuchagua viongozi wenye maadili mema watakao wasimamia bila ubaguzi.