Vikundi 17 vya watu wanaoishi na ulemavu katika Kaunti ya Nakuru vimefadhiliwa Sh1.5m zitakazowasaidia kujiinua maishani kutoka kwa serikali kuu, chini ya mwavuli wa baraza la kitaifa la walio na ulemavu (National Council For People With Disabilities).
Zoezi hilo lililoongozwa na Julius Ndwiga, ambaye ni afisa mkuu wa mipangilio katika afisi hiyo linanuia kuwafaa takriban walemavu wanne kutoka kila eneo bunge katika Kaunti ya Nakuru na hivyo kuweza kuyabadili na kuyaimarisha maisha yao ya baadaye.
Akizungumza na wanahabari mjini Nakuru siku ya Jumatano, Ndwiga alisema kuwa afisi yao imeweza kutoa hela za kuanza miradi ya kujiimarisha kiuchumi kwa vikundi 17 huku kila kikundi kikipokea Sh50,000 sawia na kutoa hundi za shule kwa wanafunzi wanaotoka kwa jamii maskini na walio na changamoto za ulemavu.
“Hii leo tuko hapa mjini Nakuru kutoa hundi kwa makundi ya watu wanaoishi na ulamavu kuwawezesha kujimudu maishani. Tumetoa hundi kwa makundi 17. kila kundi limepokea Sh50,000 kuanzisha biashara kwa wanachama wao. Pia tumetoa hundi nane kwa shule zenye thamani ya Sh600,000 ili fedha hizo zitumiwe na watoto kutoka familia maskini na wanaohitaji msaada wa kuendelea na masomo yao,” alisema Ndwiga.
Ndwiga alisema kuwa anatumai kwamba kupitia kwa mradi huo, wataweza kuwahamasisha wanaoishi na ulemavu ili waweze kuwa watu wa kujitegemea na haswaa katika kujitafutia fedha za kutosheleza mahitaji yao ya kila siku.
Emmah Mbugua, ambaye ni mwakilishi mteule wa walio na ulemavu katika Kaunti ya Nakuru aliwasihi waliozipokea hela husika kuzitumia kwa kujinufaisha kwa maisha yao ya baadaye.
Mbugua aliwasihi wanaoishi na ulamavu katika Kaunti ya Nakuru kujitokeza katika zoezi litakaloandaliwa kwenye wadi zote chini ya jimbo na kuweza kutambulika, sawia na kunufaika na hela zilizotengwa na serikali ya Kaunti.