Serikali ya Kaunti ya Nyamira imetangaza kuwa itaanzisha mikakati yakuwapa wanaoishi na ulemavu vitimagurudumu kabla yakutamatika kwa mwaka huu.
Akizungumza katika eneo la Chepilat siku ya Jumatatu, katibu wa afya kwenye Kaunti ya Nyamira Douglas Bosire alisema kuwa serikali ya kaunti hiyo tayari ishanunua viti 200 zitakazokabidhiwa walemavu ambao wamesajiliwa na idara ya watu wanaoishi na ulemavu.
Bosire alisema kuwa serikali ya kaunti hiyo ililazimika kurejesha vitimagurudumu hivyo kwa aliyekuwa akizitengeneza ili kuzitengeza vizuri kuhakikisha kuwa zinawafaa watakaozipokea.
"Serikali ya kaunti tayari imenunua viti 200 ambavyo tutavipokea kabla ya mwisho wa mwaka huu. Viti hivyo vitakabidhiwa kwa waliojisajili,” alisema Bosire.
Bosire aidha aliwahimiza watu wanaoishi na ulemavu ambao bado hawajajisajili kuhakikisha kuwa wamefanya hivyo ili idara ya afya izingatie matakwa yao.
Alisema kuwa kujisajili kwao kutawafaidi pakubwa kwa vile kutawawezesha kupokea huduma mbalimbali.
"Serikali ya kaunti iko tayari kufanya kazi na watu wote bila ubaguzi wa aina yoyote. Baadhi ya watu wanaoishi na ulemavu hawajachukua hatua yakujisajili ila nawahimiza wafanye hivyo ili wafaidi katika siku za usoni,” alisema Bosire.