Share news tips with us here at Hivisasa

Shughuli za kawaida zilitatizika kwa muda katikati mwa mji wa Nyamira baada ya muungano wa watu wanaoishi na ulemavu NAPD kuandamana kulalamikia kutengwa na serikali ya kaunti kwenye utoaji wa nafasi za kazi.

Wakihutubia wanahabari nje ya afisi za bunge la kaunti ya Nyamira walipokwenda kuwasilisha lalama zao kwa spika wa kaunti Joash Nyamoko, ambaye hakuwemo afisini mwake siku ya Jumatatu, watu hao wanaoishi na ulemavu walidaia kuwa serikali ya kaunti hiyo imekuwa ikiwatenga kwenye shughuli mbalimbali.

Mwenyekiti wa watu wanaoishi na ulemavu Evans Omwando alidai kuwa wakuu wa serikali ya kaunti hiyo hawaheshimu katiba katika kuwahusisha walemavu kwenye shughuli muhimu zinazoendelezwa katika kaunti hiyo.

"Ni jambo lakushangaza kwamba wakuu wa kaunti hii hawaheshimu katiba kwa kutubagua nakututenga kwenye nafasi za kazi,” alisema Omwando.

Mwenyekiti wa muungano huo wa zaidi ya wanachama 1500 aliuliza ni kwa nini kaunti hiyo isiwaajiri kazi huku ikizingatiwa kuwa wengi wao wamehitimu kwenye taaluma mbalimbali.

"Huu ni ubaguzi wa hali ya juu kupata kwamba tunaweza tengwa kwenye uajiri wa kazi za umma ilhali wengi wetu ni wataalam wa taaluma mbalimbali,” alisema Omwando.

Kwa upande wake, katibu mratibu wa chama hicho cha walemavu Jared Wilberforce alisema kuwa wakati umewadia kwa walemavu kutafuta haki yao.

“Wakati umefika kwa sisi walemavu kutafuta haki yetu kwa maana kwa muda mwingi wakuu wa kaunti hawajakuwa wakiona umuhimu wetu katika kuchangia uchumi wa kaunti hii,” alisema Wilberfoce.

Aidha walemavu hao wamemwomba gavana wa kaunti hiyo John Nyagarama kusuluhisha matatizo yao mara moja la sivyo wapeleke kesi mahakamani kuishtaki serikali ya kaunti kwa ubaguzi.

"Tunamwomba gavana wa kaunti hii kushughulikia matatizo yetu kwa haraka na iwapo hilo halitaafikiwa, tutapeleka kesi mahakamani kuishtaki serikali ya kaunti hii kwa ubaguzi,” alisema Wilberfoce.