Walemavu katika kaunti ya Kisii wameshauriwa kujitokeza na kujiandikisha katika vikundi ili kupata mgao wao wa kifedha kutoka kwa serikali.
Wito huo umetolewa baada ya kubainika kuwa idadi nyingi ya walemavu bado hawajajisajili kwenye vikundi ili kupata mgao wao kutoka kwa serikali licha ya kuwa kuna hazina ambayo ni ya kusaidia walemavu.
Mwenyekiti wa walemavu katika kaunti ya Kisii Isaac Rogito alisema ni vizuri kwa kila mlemavu kujiandikisha kwa kikundi cha walemavu ili apate kusaidiwa na serikali.
“Walemavu wale ambao wamejiunga kwa vikundi vyao tayari wamepokezwa pesa ambazo zitawasaidia maana serikali ya kitaifa imetenga millioni 1.7 katika kaunti yetu ili kusaidia walemavu kujiendeleza na kujiimarisha kimaisha,” alisema Rogito.
“Naomba wale ambao bado hawajajiunga kwa vikundi kufanya hivyo ili kupata usaidizi kutoka kwa serikali," aliongeza Rogito.
Aidha, Rogito aliomba walemavu wanapojiunga kwa kikundi chochote wasizidi watu 20 kwani kila kikundi kinastahili kuwa na watu 15 hadi 20 ili kusaidiwa na serikali.