Idadi kubwa ya walemavu katika eneo bunge la Nyaribari Chache kaunti ya kisii wamenufaika kutoka kwa serikali ya kitaifa baada ya kusajiliwa na kununuliwa kadi za matibabu za NHIF.
Akizungumza nasi siku ya Jumatano mjini Kisii afisa anayesimamia walemavu hao Kennedy Okong’o alisema kuwa walemavu hao walifaidika baada ya kununuliwa kadi hizo ili kupokea matibabu bila malipo.
Aidha, afisa huyo alisema baadhi ya wazee ambao wamezeeka nao walijumuishwa kwa shughuli hiyo ambapo watanufaika na shughuli hizo za matibabu.
“Kwa sasa zaidi ya watu 600 ambao ni walemavu na wazee katika eneo bunge la Nyaribari Chache wamenufaika kutoka kwa serikali kuu baada ya kununuliwa kadi za NHIF," alisema Okong’o.
“Serikali inahitaji watu hao kutosumbuka wanapotafuta matibabu katika hospitali mbalimbali humu nchini ” aliongeza Okong’o.
Aidha, afisa huyo alisema kuwa watu hao hupokea shillingi 2,000 kila mwezi kando na matibabu hayo ili kujiendeleza kimaisha.