Mahakama ya Mombasa imewaachilia huru walimu 12 wa Shule ya msingi ya Star of the Sea, waliokuwa wanakabiliwa na mashtaka ya kuhusika katika wizi wa mtihani wa kitaifa wa KCPE.
Walimu hao wanadaiwa kupatikana na karatasi za mitihani ya somo la hisabati, kiingereza na somo la insha katika mtandao wa Whatsapp, mwaka wa 2015.
Akitoa uamuzi huo siku ya Jumatano, Hakimu Edgar Kagoni alisema nakala za mitihani hiyo hazikuwa na nembo ya Baraza la mitihani nchini KNEC.
“Karatasi hizo hazikuwa na nembo ya baraza la KNEC kwa hivyo ni vigumu kubaini iwapo zilitoka kwa baraza hilo,” alisema Hakimu Kagoni.
Aidha, hakimu huyo alisema kuwa afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma ilikosa kuwasilisha ushahidi wa kutosha.
“Afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma haikuwasilisha ushahidi wa kutosha ikiwemo kuleta ratiba ya mitihani kutoka baraza la mitihani nchini,” alisema Kagoni.
Hata hivyo, mahakama imeagiza washukiwa hao kuregeshewa simu zao ambazo zilikuwa zimezuiliwa.