Kongamano la walimu wakuu nchini ambayo imekua ikiendelea jijini Mombasa kwa muda wa wiki moja imefika kileleni huku walimu waliomakinika kazini wakituzwa.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akiongoza hafla hiyo siku ya Ijumaa, mkurugenzi mkuu wa Tume ya kuajiri walimu nchini TSC Nancy Macharia alitoa wito kwa washindi wa tuzo mbali mbali kutumia fursa hiyo kutoa mafunzo kwa wenzao ili kufaidi wanafunzi.

Mwalimu mkuu wa Shule ya upili ya Emining ambayo iko katika Kaunti ya Baringo Solomon Koech ndiye aliyeibuka mshindi katika tuzo ya mwalimu mkuu bora wa mwaka wa 2016.

Koech ambaye amehudumu kama mwalimu mkuu wa shule hiyo kwa muda wa miaka mitano alisema kuwa ushindi huo umetokana na ushirikiano wake na walimu wengine.

Katika kitengo cha mwalimu bora mwaka wa 2016, Lucy Mugo, mwalimu wa Kiswahili katika Shule ya upili ya wasichana ya Karatina aliwabwaga wenzake kutoka kaunti zingine na kuibuka mshindi baada ya somo lake kupata alama 89.46 katika mtihani wa kitaifa uliofanywa mwaka jana.

Tuzo hiyo ya mwalimu mkuu bora na mwalimu bora hutolewa kila mwaka na Tume ya TSC katika kongamano la walimu wakuu na hutumiwa katika kuwapandisha cheo walimu hao.