Katika hatua inayolenga kuhakikisha kuwa mradi wa vipakatalishi unafaulu katika shule za umma kote nchini, serikali imeweka mikakati ya kutoa mafunzo kwa walimu wote wa shule za msingi ili kurahisisha utumiaji wa vipakatalishi hivyo.
Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatano, Mkurugenzi wa Elimu katika Kaunti ya Mombasa, Abdikadir Kike, alisema kuwa serikali ilianza kutoa mafunzo hayo tangu mapema mwaka 2015 na kuwa zoezi hilo litaendelea kote nchini.
“Serikali itahakikisha kuwa walimu wetu wanafundishwa namna ya kuvitumia vipakatalishi hivyo ili waweze kuwaelekeza wanafunzi kwa namna inayofaa,” alisema Kike.
Aidha, Kike alisema kuwa serikali itaimarisha usalama katika shule zote za umma nchini ikiwemo kuunganisha stima ili kutoa ulinzi wa kutosha kuzuia vipakatalishi hivyo kuibwa.
Awamu ya kwanza ya mradi wa kutoa vipakatalishi katika shule za msingi za umma ilianza siku ya Jumanne ambapo takribani shule 150 kutoka kaunti zote nchini zilinufaika.
Jumla ya shule 18 katika ukanda wa Pwani zilipokea vipakatalishi hivyo huku shule tatu za Kaunti ya Mombasa zikinufaika na mradi huo.