Huenda walimu wa shule za chekechea wasiokuwa na vibali wakafutwa kazi ili kupisha wale waliohitimu kutwaa nafasi zao.
Haya ni kwa mujibu wa afisa mshirikishi wa huduma za walimu wa chekechea katika kaunti ndogo ya Rabai Josphine Maraga, ambaye amesema kwamba idadi kubwa ya walimu wanaohudumu kwa sasa wanakosa vyeti vinavyoonyesha kuhitimu kwao.
Akizungumza na wazazi huko Ruruma wakati wa ufunguzi wa shule moja ya chekechea, Maraga alisema kwamba walimu hao wanapaswa kuwa na angalau cheti kinachoonyesha kuhitimu shule ya upili ndiposa waweze kuhudumu kama walimu wa chekechea.
Maraga pia amewataka wazazi wa kaunti ndogo ya Rabai kushirikiana na idara ya elimu katika eneo hilo ili kuona kwamba watoto wao wanaanza masomo pindi tu watakapohitimu miaka mitatu.
“Idara ya elimu katika eneo hili inaazimio la kuongeza vituo vya shule za chekechea ili kukidhi idadi kubwa ya watoto katika eneo hili,” alisema Maraga.
Aidha, msimamizi wa eneo la Rabai Mulewa Katana, alitaja tatizo la kutojua kusoma na kuandika kama adui mkubwa eneo zima la Pwani, anayechangia kudorora kwa maendeleo katika eneo hilo.
Mulewa aliwataka wakazi wa Rabai kukumbatia umuhimu wa elimu ili kukumbana na janga hilo, huku akiwataka wazazi kushirikiana na walimu wa shule za chekechea ili kuona kwamba watoto wao wanalikabili tatizo hilo wakiwa wachanga.