Walimu wote wa Muungano wa Walimu Kenya (KNUT) tawi la Gucha wameaswa kutotia sahihi kandarasi za utendakazi wao hata iwapo watapokea vitisho.
Wameombwa wasilegeze kamba hadi maafisa wakuu wa chama hicho watakapo toa ripoti kamili kuhusu jambo hilo.
Katibu wa chama hicho tawi la Gucha Lucy Machuki alikiri kuwa msimamizi wa Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) tawi la kaunti ya Kisii Martine Munde amekuwa akiwatishia walimu kutia sahihi hizo ila amewaomba walimu kutotishika.
Machuki alisema tume ya TSC bado haijaelewana na chama cha KNUT dhidi ya sahihi hizo wanazohitajika kusahihisha na kusema maafisa wakuu wa chama hicho akiwemo Katibu mkuu Willson Sossion na mwenyekiti watatoa ripoti kamili kuhusu swala hilo.
“Naomba walimu walio chini ya mwavuli wa KNUT tawi la Gucha na kaunti nzima ya Kisii kutokubali kutia sahihi ya utendakazi hadi ripoti kamili itolewe kutoka kwa wakuu wetu na pasiwena jazba yeoyote ile,” alisema Machuki.