Wanafunzi wa Shule ya Upili ya Songhor ambao walifanya vizuri kwenye jaribio la Kiswahili ya Wilaya ya Muhoroni la hivi punde walituzwa na Shirika la Habari la Nation Media Group fulana za Taifa Leo na vitabu za Kiswahili kupitia Chama cha Waandishi wa Kiswahili cha Taifa, (WAKITA).
Shule hiyo iliongoza kwenye jaribio la somo la Kiswahili kwa shule za kanda hiyo wakati wanafunzi wake watano walipopata alama mia moja. Kwa mujibu wa msimamizi wa sehemu hiyo ya jaribio la msimu huu Nicholas Omala, kiwango hicho ni cha kwanza cha juu kushuhudiwa kwa muda wa miaka mitano sasa.
“Shule hii imeweka rekodi ya kipekee msimu huu ikilinganishwa na matokeo ya majaribio ya hapo awali ya miaka mitano iliyopita ambapo tulikua na rekodi ya wanafunzi watatu kutoka Shule ya St. Stephen ilioko mjini Muhoroni waliopata alama mia moja,” alisema Omala.
Akihutubu wakati wa hafla iliyoandaliwa shuleni humo mnamo siku ya Jumatatu, washirikishi wa WAKITA eneo hilo, Osborne Manyengo aliahidi kutoa zawaidi zaidi kwa wanafunzi watakaopita somo hilo kwenye mtihani mkuu ujao wa KCSE, huku akihimiza wanafunzi kutia bidii kwenye somo hilo ambalo linajenga utaifa wa nchi hii, ikizingatiwa kuwa Kiswahili ndicho lugha ya kitaifa.
Washirikishi wa WAKITA ambao waliandamana na Manyengo pia walihimiza walimu kuzingatia somo hilo kwa kuwashirikisha wanafunzi kwenye mijadala ya Kiswahili, wakisema kwamba wanafunzi wanaposhiriki mijadala mara kwa mara watakua na uzoefu katika semi za Kiswahili sanifu.
“Semi za kisheng zinaendelea kuwanasa vijana wetu na huu ni wakati mwafaka kwa walimu kuhakikisha kwamba wanakikomboa kizazi cha sasa kutoka katika ubeberu wa sheng,” alisema Ester Riziki, mwanachama wa WAKITA.