Mwalimu mkuu wa Shule ya Upili ya Chumani amesema kuwa zaidi ya wanafunzi mia moja hamsini kutoka shule za upili katika eneo la Pwani hukosa kurudi shuleni kuendelea na masomo pindi tu wanapoenda likizoni.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza wakati wa kupokea msaada wa sare za shule kwa wanafunzi kutoka kwa shirika lisilo la kiserikali la 'GAPEKA Childrens Home', Racheal Kazungu alisema kuwa wanafunzi wasiojiweza nyumbani hukosa kurudi shuleni na badala yake kuishia mijini kujitafutia riziki kutokana na hali ya umaskini nyumbani kwao.

Kazungu aliongeza kuwa kila muhula unapoanza, idadi ya wanafunzi wanaorejea kwenye masomo ya muhula mpya hupungua kwa kiasi kikubwa, huku sababu kuu ikiwa kukosa baadhi ya vitu muhimu kama vile sare za shule, matatizo ya nyumbani, miongoni mwa sababu nyengine zinazochangia wanafunzi kuacha shule.

Kauli ya Kazungu iliungwa mkono na mwalimu mkuu wa Shule ya Upili ya Mariakani James King’ori ambaye alisema kwamba katika shule yake, wanafunzi zaidi ya thelathini hukosa kurudi shuleni kila mwaka kutokana na hali ngumu ya maisha.

“Wanafunzi hao hukosa mahitaji muhimu ya nyumbani ambayo inapelekea wengi wao kuanza kazi ya kuendesha bodaboda ili kukimu mahitaji ya familia zao nyumbani,” alisema King’ori.

Hata hivyo, wametoa wito kwa mashirika mbalimbali ikiwemo ya serikali pamoja na yale ya kibinafsi kuwasaidia wanafunzi kwani wengi wao huwa werevu darasani ila huishia kutafuta kazi za kijungu jiko.