Katibu wa chama cha Knut tawi la Mombasa, Dan Aloo, amethibitisha kuwa walimu waliosahihisha mitihani ya kitafa ya mwaka jana tayari wameanza kupokea malipo yao.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kwenye mahojiano na mwandishi huyu afisini mwake siku ya Jumatano, Aloo alisema kuwa walimu waliousimamia mtihani wa darasa la nane KCPE, walianza kulipwa wiki hii huku wale walioutahini mtihani wa kidato cha nne KCSE,  wakitarajiwa kupokea malipo yao juma lijalo.

“Asilimia 70 ya walimu wa shule za msingi waliousimamia mitihani ya kitaifa mwaka uliopita tayari wamepokea malipo yao. Wale ambao hawajapokea labda ni kutokana ya tashwishi kwenye simu zao kwa kuwa wanalipwa kwa njia ya simu. Ningependa kuwasihi wazuru afisi za Knec zilizoko karibu kubaini tatizo liko wapi,” alisema Aloo.

Hata hivyo, Aloo ameeleza hofu yake kuwa huenda walimu wakasusia kuusimamia mtihani wa mwaka huu kufuatia hatua ya Baraza la mtihani nchini Knec kuchelewesha malipo yao.

“Hivi karibuni Knec itawahitaji walimu tena kuusimamia mtihani wa mwaka huu. Nahofia huenda wakadinda kuutikia wito huo sababu wengi wamelalamika sana,” aliongeza Aloo.

Kulingana na Aloo, Knec ilifaa kuwalipa walimu hao miezi mitatu baada ya zoezi la kusahihisha mtihani kutamatika na wala sio miezi tisa baadaye kama ilivyoshuhudiwa mwaka huu.