Walimu katika Shule ya msingi ya Khadija wamempongeza Rais Uhuru Kenyatta kwa kupitisha sheria ya kuorodheshwa kwa shule kulingana na matokeo ya mitahani ya kitaifa.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza siku ya Alhamisi, mwalimu mkuu wa shule hiyo Bwana Kibuga, alisema takribani nusu ya walimu Pwani wamekuwa wakisubiri kwa hamu kupitishwa kwa sheria hiyo.

Kibuga alisema kuwa hatua hiyo itasaidia kuinua viwango vya elimu kote nchini kwani itawasaidia watahiniwa kujua namna wanavyofanya kwenye mitihani hiyo kwa kujilinganisha na shule zingine.

Sheria hiyo ambayo ilifutiliwa mbali na aliyekuwa Waziri wa Elimu Professa Jacob Kaimenyi sasa italilazimu Baraza la mitihani nchini KNEC, kurudia zoezi la kuorodhesha shule na watahiniwa kwa mujibu wa matokeo ya mitihani hiyo.

Hata hivyo, Waziri wa Elimu Fred Mating’i amesema kuwa hatua hiyo inachangia ongezeko la visa vya udanganyifu na wizi wa mitihani kwa kuwa kila shule itahitaji kujiweka katika nafasi bora kwenye orodha ya matokeo.

Kauli hiyo imepingwa vikali na mwalimu Kabugua aliyesema kuwa kama kutaibuka visa vya wizi wa mitihani, basi anayepaswa kuwajibikia tatizo hilo ni maafisa wakuu katika baraza la mitihani.

Kwa upande wao, wanafunzi wa Shule ya upili ya Junda iliyoko Mtaa wa FrereTown wamesema Rais Kenyatta alifanya jambo la busara kuidhinisha sheria hiyo.

Walisema kuwa ikiwa watahiniwa wataandikisha matokeo mazuri, basi ni lazima wajue wanaoshindana nao ili wajue sehemu ya kutilia nakshi ama ya kusoma zaidi ili kuweza kuwashinda wenzao.

Aidha, kwa mujibu wa naibu mwalimu mkuu wa Shule ya Junda Erastus Chondo, hakuna mwalimu wala mwanafunzi anayeweza kuiba mtihani shuleni ila ni maafisa wakuu ambao hutekeleza biashara hiyo.

Mwalimu huyo hata hivyo amesema tangu miaka ya hapo awali, shule zimekuwa zikiratibiwa kwa mujibu wa matokeo na hakukuwa na visa vyovyote vya udanganyifu.

Chondo alisema kuwa hatua hiyo inatokana na kuenea kwa ufisadi katika baadhi ya asasi za serikali.

Sheria hiyo sasa imetoa mwelekeo mpya kwa baraza la mitihani nchini kuanza mchakato wa kuorodhesha shule katika masuala mbalimbali ikiwemo elimu na michezo ili kusaidia kuboresha sekta zote na hata kuzitambulisha sekta hizo.