Onyo kali imetolewa kwa walimu wanaoendeleza elimu ya ziada wakati wa likizo kwamba watachukuliwa hatua za kisheria.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akitoa onyo hilo mjini Mombasa siku ya Jumatatu,  mkurugenzi wa elimu katika kaunti ya Mombasa Abdikadri Kike amedokeza kwamba hata licha ya serikali kupiga marufuku masomo ya ziada bado kuna baadhi ya walimu wanaoendeleza masomo hayo kwa njia ya siri.

Kike ameshikilia kwamba lazima amri ya serikali ifuatwe kikamilifu, na akawaomba walimu wanaoendeleza masomo ya ziada kwa njia ya siri kukomesha tabia hiyo mara moja kabla ya serikali kuwachukulia hatua za kisheria.

"Walimu wanaoendeleza masomo ya ziada wakati wa likizo tunawaomba kusitisha taibia hiyo mara moja kabla ya serikali kuwachukulia hatua kali za kisheria kwani hatua hiyo ilipigwa marufuku na serikali," alisema Kike.

Kauli ya mkurugenzi huyo inajiri baadaya kuweko na fununu kwamba kuna baadhi ya walimu katika kaunti ya Mombasa wanaendeleza masomo ya ziada kwa njia ya siri licha ya serikali kuyapiga marufuku.