Baada ya mradi wa kufunza walimu madarasa ya kutumia tarakilishi kukamilika, mkururugenzi wa elimu katika kaunti ya Kisii amewataka walimu wote waliofuzu kuendelea kufanya mazoezi ya utekelezi hata baada ya mradi huo kufika mwisho ili wawe na ujuzi wa kutosha wakati wataanza kuwafunza wanafunzi.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Kwenye mahojiano katika ofisi siku ya Ijumaa, mkurugenzi huyo, Richard Chepkawai, aliweka wazi umuhimu wa walimu hao kuendelea kujifunza jinsi ya kutumia kompyuta, ili kuhimarisha ufahamu wao katika kutumia mitambo hiyo ya kuwafunza wanafunzi wa darasa la kwanza.

Mpango huu umekuwa ukiendelea katika kaunti zote nchini, hii ikiwa mojawapo ya miradi ya serikali ya Jubilee kuwakomaza walimu wa shule za umma za msingi kiujuzi watakavyozitumia kompyuta kuwaelimisha wanafunzi, ambapo awamu ya kwanza inalenga wanafunzi walioko katika darasa la kwanza.

Chepkawai alionyesha furaha yake kuhusiana na ushirikiano ulionyeshwa na walimu hao, ambapo aliwashukuru walimu hao huku wakijiandaa kumaliza masomo hayo.

Aidha, mkurugenzi huyo aliwapongeza walimu ambao ni wazee na wana umri mkubwa kwa kukumbatia mradi huo wa kutumia kompyuta hizo.

“Nimeona fahari kubwa kwa walimu walioshiriki katika zoezi hili tangu lianze hadi sasa linapoelekea kukamilika na haswa wale walimu ambao walikuwa na umri mkubwa wameonyesha ari kubwa ya kutumia mitambo hii,” alihoji    Chepkawai.

Mkurugenzi pia aliwaomba wazazi wa kaunti hiyo ya Kisii kushirikiana na walimu ili kuimarisha viwango vya elimu katika eneo lote la Kisii.