Wakazi wa Kaunti ya Nyamira wamewaomba walimu kuwafungulia watoto kutoka shuleni mapema ikiwa kuna dalili ya mvua ili kuepusha visa vya watoto kusombwa na maji mvua inaponyesha.
Hii ni baada ya visa vingi vya watoto kusombwa na maji ya mvua kuongezeka kila wakati katika sehemu mbali mbali za Kaunti ya Nyamira, jambo ambalo limewalazimu wakazi hao kuomba walimu wa shule za msingi kuwafungulia watoto pindi mvua inapoanyesha ishara ya kunyesha.
Wakizungumza na Waandishi wa habari siku ya Jumatatu katika uwanja wa Shule ya Msingi ya Riyabe ilioko katika Kaunti ya Nyamira, wakazi hao ambao wengi wao ni wazazi wakiongonzwa na Lydiah Maiko walisema ikiwa visa vya kupoteza maisha ya watoto kupitia maji ya mvua vinahitajika kupunguzwa, sharti watoto wafunguliwe mapema kutoka shuleni ili mvua itakapoanza kunyesha impate kila mtoto amefika nyumbani.
“Tunaomba walimu wasikie kilio chetu kama wazazi maana watoto wetu wanaendelea kupoteza maisha yao kila wakati kupitia mfuriko. Sasa tunaomba walimu haswa wa shule za msingi wawe wanawafunguliwa watoto wetu mapema lakini wakati hamna mvua watawafungulia wakati ule umepitishwa na serikali kuu kupitia Wizara ya Elimu,” alidokeza Marizellah Kemunto Bosire, mkazi pia mzazi wa shule ya Riyabe.
Aidha, wakazi hao pia waliomba Gavana wa kaunti hiyo John Nyagarama kuhakikisha kuwa viwango vya elimu vimeinuka katika kaunti ya Nyamira.
Shule nyingi katika kaunti hii zina upungufu wa walimu ndio maana tunamuomba gavana wetu awasiliane na serikali ya kitaifa iongeze walimu,” alisema Isaac Nyaruri, mkaazi pia mzazi wa shule hiyo.